Unganishwa

Search the region

22731 stories

Business · Issa Michuzi

RAIS SAMIA KUFUNGUA MKUTANO UWEKEZAJI MADINI,SERIKALI YAJIVUNIA

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TIMC), huku Serikali ikijivunia mafanikio ya sekta hiyo yanayooneshwa na kuongezeka kwa mchango wake katika Pato la Taifa, mapato na mauzo ya madini nje ya nchi. Mkutano huo utafanyika kuanzia Novemba 19 hadi 21, mwaka huu, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, ukiwa na washiriki 1,700 kutoka ndani na nje ya nchi ambao tayari wamethibitisha kushiriki. Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo yametokana na juhudi za Serikali kuboresha usimamizi wa rasilimali za madini, kuongeza mapato, kuvutia uwekezaji na kuwawezesha wachimbaji wadogo. Amefafanua mkutano huo ni wa saba tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019 na utatoa fursa ya kujadili mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo pamoja na fursa mpya za uwekezaji, hususan katika kuongeza thamani ya madini nchini. Amesema mkutano huo utafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Madini Yaliyoongezwa Thamani, Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi.” Ameongeza kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha uwekezaji katika uchakataji na uongezaji thamani wa madini ndani ya nchi ili sekta hiyo izalishe manufaa makubwa zaidi kwa uchumi na wananchi. Akielezea mafanikio ya sera ya ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini, amesema ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka kwa wazalishaji na watoa huduma wa ndani umeongezeka kutoka Sh.bilioni 884.09 mwaka 2010 hadi Sh.trilioni 5.2 mwaka 2025. Amesema ongezeko hilo linaonesha namna shughuli za uchimbaji madini zinavyoendelea kufungua fursa za kibiashara kwa kampuni za ndani na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta hiyo. Katika hatua nyingine, amesema mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeongezeka hadi kufikia asilimia 10.3 mwaka 2025, kutoka asilimia 7.8 mwaka 2024. Waziri Mavunde amesema ukuaji huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa thamani ya madini yanayouzwa nje ya nchi, ambayo yalipanda kutoka Dola za Marekani bilioni 4.12 mwaka 2024 hadi bilioni 5.46 mwaka 2025. Kwa mujibu wa Waziri huyo, ongezeko hilo linaashiria kuimarika kwa nafasi ya sekta ya madini katika uchumi wa Taifa na uwezo wake wa kuchangia upatikanaji wa fedha za kigeni. Kuhusu mapato ya Serikali, amesema yameongezeka kutoka takribani Sh bilioni 526 katika mwaka wa fedha 2020/2021 hadi Sh trilioni 1.39 katika mwaka wa fedha 2025/2026. “Mafanikio hayo yanatokana na kuimarishwa kwa usimamizi wa shughuli za madini na mifumo ya ukusanyaji wa mapato, hatua iliyowezesha Serikali kunufaika zaidi na rasilimali hizo.” Akizungumzia ajira, Waziri Mavunde amesema hadi Aprili 2025, sekta hiyo ilikuwa imetoa ajira rasmi 10,874, ambapo asilimia 97.4 zilikuwa za Watanzania. Amesema takwimu hizo zinaonesha mchango wa sekta ya madini katika kupanua fursa za ajira kwa wananchi, kuongeza kipato na kukuza shughuli nyingine za kiuchumi zinazohusiana na uchimbaji na biashara ya madini. Hivyo amesema mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wawekezaji, wadau wa sekta ya madini na Serikali kujadili namna ya kuongeza uwekezaji, kuimarisha ushiriki wa wazawa na kuhakikisha rasilimali za madini zinachangia zaidi katika maendeleo ya Taifa.

Tue, 17 Nov 2026 16:01:17 +0000
National · Issa Michuzi

SHULE YA SEKONDARI VUGA BAZO YANUFAIKA NA HOSTELI, VYOO 14 KUPITIA SHIRIKA LA BETTER WORLD CANADA

Wadau wa maendeleo waombwa kuongeza vitanda, nyumba za walimu na miundombinu mingine ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuinua ufaulu wa wanafunzi. Na Mwandishi Wetu, Bumbuli SHULE ya Sekondari Vuga Bazo iliyopo Kata ya Soni, Halmashauri ya Bumbuli, Mkoa wa Tanga, imenufaika na ujenzi wa hosteli ya wavulana pamoja na matundu 14 ya vyoo, hatua inayotarajiwa kuondoa changamoto ya uhaba wa vyoo na umbali mrefu wa safari kwa wanafunzi. Mradi huo umefadhiliwa na Shirika la Better World Canada kwa kushirikiana na Shirika la Vuga Development Initiative kutekeleza mradi huo kwa kwa gharama ya shilingi Milioni 93. Akizungumza kuhusu manufaa ya mradi huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Vuga Bazo, Mathias Chambwite, alisema shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa matundu ya vyoo pamoja na kukosekana kwa hosteli kwa wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali. Alisema kabla ya msaada huo, shule ilikuwa na matundu 12 ya vyoo, hali iliyosababisha wanafunzi kusubiri kwa muda mrefu ili kupata nafasi ya kutumia vyoo kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi. Chambwite alisema kwa sasa shule imeongezewa matundu 14 na kufanya jumla ya matundu ya vyoo kufikia 26, ambayo yanakidhi mahitaji ya wanafunzi 390, wakiwemo wasichana 210 na wavulana 180. Alisema ujenzi huo umeondoa changamoto iliyokuwa ikiathiri mazingira ya kujifunzia na kwamba uwepo wa hosteli utawasaidia wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali kupata nafasi nzuri ya kulala, kupumzika na kujisomea. “Tunawashukuru sana wafadhili wa Better World Canada kwa kutusaidia kujenga hosteli na vyoo. Changamoto kubwa tuliyokuwa nayo ilikuwa miundombinu, lakini kupitia msaada huu tunaamini wanafunzi watapata mazingira mazuri ya kusoma na kufikia malengo yao,” alisema Chambwite. Alisema kwa upande wa Serikali, shule hiyo haina changamoto kubwa ya walimu, kwani ina walimu wa kutosha, walimu wa masomo ya sayansi pamoja na mtaalamu wa maabara. Hata hivyo, aliwaomba wadau wengine kuendelea kuisaidia shule hiyo, hasa kwa kuongeza vitanda vya hosteli, kujenga jengo la utawala na kuongeza nyumba za walimu ambazo bado hazitoshelezi mahitaji ya watumishi waliopo. Alisema shule hiyo ina idadi kubwa ya wanafunzi wa kike ambao wanahitaji mazingira bora ya kujifunzia ili waweze kutimiza ndoto zao, akibainisha kuwa jitihada za kuwawezesha wasichana kuendelea na masomo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zilizokuwa zikiwakwamisha hapo awali. Mratibu wa Shirika la Vuga Development Initiative, Rama Kaoneka aliwataka watu walisoma katika shule hiyo watambue nyumbani ni nyumbani hivyo ni vizuri wakumbuke na kurudisha fadhila zao ili wanafunzi waweze kusoma sehemu nzuri. Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Vuga, Jumaa Dhahabu, alisema wanamshukuru Mungu na wafadhili kwa kufanikisha ujenzi wa hosteli hiyo, akieleza kuwa awali wanafunzi walikuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita 18 kwenda na kurudi shuleni kila siku. Alisema hali hiyo ilikuwa ikiathiri maendeleo ya kitaaluma ya wanafunzi na kuchangia matokeo yasiyoridhisha, kutokana na uchovu waliokuwa wakipata wakati wa safari. “Tunawashukuru sana wafadhili kwa kuona changamoto iliyokuwa ikiikabili shule yetu. Tunaamini hosteli hii itabadilisha matokeo ya wanafunzi kwa sababu sasa watapata nafasi ya kukaa karibu na shule na kutumia muda mwingi kujisomea,” alisema Dhahabu. Aliwapongeza Shirika la Better World Canada pamoja na Kaoneka, Mkurugenzi wa Shirika la Vuga Development Initiative, kwa juhudi zake za kuunganisha jamii na wafadhili, huku akitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia ujenzi wa mabweni zaidi ili wanafunzi wengi waweze kupata huduma hiyo. Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli, Magreth, aliishukuru Better World Canada kwa kuendelea kushirikiana na halmashauri katika sekta za elimu na afya, akizitaja kuwa ni maeneo muhimu yanayogusa maisha ya wananchi. Alisema pamoja na hosteli ya wavulana na matundu 14 ya vyoo, halmashauri inaomba wadau hao waendelee kusaidia miradi mingine ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa hosteli ya wasichana katika shule hiyo. Aidha, alisema halmashauri inahitaji shule nyingine ya sekondari yenye masomo ya sayansi kwa ngazi ya kidato cha tano na sita, ili kuwasaidia wanafunzi wanaofaulu kidato cha nne lakini wanashindwa kuendelea na masomo katika maeneo ya mbali kama Arusha, Kigoma na Dar es Salaam kutokana na changamoto za kifedha kwa wazazi. Alisema upatikanaji wa shule hiyo utasaidia wanafunzi wengi kuendelea na masomo ya sayansi, kufikia elimu ya juu na baadaye kuwa wataalamu watakaolisaidia eneo hilo. Pia aliomba msaada wa ujenzi wa jengo la utawala na upatikanaji wa vitanda ili hosteli hiyo iweze kuanza kupokea wanafunzi kuanzia Januari mwakani. Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bumbuli, Zepahia Sumaye, aliwashukuru wafadhili na Shirika la Vuga Development Initiative kwa juhudi za kuunganisha halmashauri na wadau wa maendeleo. Sumaye alisema mchango huo ni mkubwa katika kuboresha miundombinu ya elimu, akibainisha kuwa pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali katika ujenzi wa madarasa, vyoo na hosteli, bado kuna mahitaji mengine yanayohitaji ushirikiano wa wadau. Alisema hosteli hiyo itawasaidia wanafunzi kupata sehemu salama ya kulala, kupumzika na kujisomea, hivyo kuongeza uwezekano wa kufanya vizuri katika masomo yao. Aliwataka wananchi kutambua umuhimu wa maendeleo yanayoletwa na wadau na kuhakikisha wanatunza miundombinu inayojengwa kwa manufaa ya jamii. “Tunawaomba wanafunzi na wananchi wote kutunza majengo haya, hosteli na matundu ya vyoo 14 ili yaweze kudumu na kuwa na thamani. Wafadhili wanapokuja kuona matumizi mazuri ya miradi waliyoigharamia, wanapata moyo wa kuendelea kutusaidia,” alisema Sumaye. Pia alimshukuru Kaoneka kwa jitihada zake za kutafuta marafiki na mashirika ya maendeleo, akieleza kuwa ushirikiano huo umechangia kupatikana kwa miradi mbalimbali katika eneo la Bumbuli. Aidha, alimwomba Diwani wa Kata ya Vuga kuratibu harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ununuzi wa vitanda vya hosteli, huku akiahidi kuchangia katika zoezi hilo. Alisema ushirikiano kati ya Serikali, wananchi na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kuhakikisha shule hiyo inapata miundombinu inayokidhi mahitaji ya wanafunzi na kuboresha kiwango cha elimu katika eneo hilo.

Tue, 17 Nov 2026 20:28:31 +0000
Business · Issa Michuzi

MENEJA MKUU KARIAKOO: MATANGAZO YA BIASHARA MTANDAONI HAYAEPUKIKI KATIKA UFANISI WA BIASHARA

Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo CPA. Ashraph Abdulkarim amewashauri wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo kutangaza bidhaa zao mtandaoni jambo litakaloendelea kutavutia wateja wengi zaidi wa ndani na nje ya nchi. Ushauri huo umetolewa wakati wa mkutano baina ya uongozi wa shirika hilo na wafanyabiahara wa Soko soko hilo, mkutano ambao umelenga kusikiliza kero na changamoto za wafanyabiashara ili kuendelea kuboresha mazingira ya biashara katika soko hilo. Amebainisha kuwa shirika limeendelea na mipango mbalimbali ya kuvutia wateja kwa kutangaza huduma na bidhaa zinazopatikana sokoni hapo, jitihada ambazo zimekuwa na mafanikio chanya kwa kuongeza mzunguko wa watu wanakuja na kutoka sokoni hapo. Ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya teknolojia nchni, ubunifu katika kuendesha biashara ni jambo lisiloepukika, kwakuwa mtu anaweza kufanya maamuzi ya bidhaa anayoitaka akiwa nyumbani au mahali popote na kuja kuichukua au kutuma mtu aifuate kwa niaba yake. Shirika la Masoko ya Kariakoo limekuwa na utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo kila baada ya miezi mitatu kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili, kupokea mrejesho na kushirikisha shughuli mbalimbali zinazoendelea sokoni hapo ili kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwao.

Tue, 17 Nov 2026 20:31:38 +0000
Uncategorized · Issa Michuzi

DAUD YASSIN KUANZA ZIARA YA SIKU 11 KUIMARISHA CHAMA MKOANI IRINGA

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Comrade Daud Yassin, anatarajiwa kufanya ziara maalum katika wilaya zote nne za mkoa huo kuanzia Novemba 21 hadi Desemba 1, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha chama na kusogeza shughuli zake karibu na wanachama. Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na CCM Mkoa wa Iringa, ziara hiyo itaanza Novemba 21 katika Wilaya ya Iringa Mjini, kabla ya kuelekea Kilolo Novemba 23 na 24, kisha Mufindi Novemba 28 na 29, na kuhitimishwa katika Wilaya ya Iringa Vijijini Novemba 30 hadi Desemba 1, 2026. Ziara hiyo yenye kaulimbiu ya #KazinaUtuTunasongaMbele inalenga kuimarisha shughuli za chama katika maeneo mbalimbali ya mkoa, huku ikitoa fursa ya uongozi wa chama kufika katika wilaya zake zote nne kupitia ratiba hiyo maalum. Hatua hiyo inaweka msisitizo katika kuendeleza uhai wa chama, kuimarisha mshikamano na kuendeleza utekelezaji wa majukumu ya CCM katika Mkoa wa Iringa.

Tue, 17 Nov 2026 20:34:02 +0000
Uncategorized · Issa Michuzi

IRINGA YAKARIBIA LENGO LA DUNIA LA 95-95-95, UELEWA WA UKIMWI WAFIKIA ASILIMIA 94.6

Mkoa wa Iringa umeendelea kupiga hatua katika mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI (VVU), huku kiwango cha uelewa wa wananchi kuhusu ugonjwa huo kikiongezeka kutoka asilimia 86.5 hadi asilimia 94.6 ndani ya kipindi cha miaka mitano, hatua inayokaribia lengo la kitaifa la asilimia 95. Akizungumza wakati wa kukabidhi vitendea kazi vilivyobaki baada ya kukamilika kwa Mradi wa Afya Yangu Southern Project, Mkurugenzi wa mradi huo, Dkt. Denis Mzaga, amesema mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuwafikia asilimia 98 ya watu waliobainika kuwa na maambukizi na kuwaanzishia matibabu, huku asilimia 98 ya wanaotumia dawa za kufubaza virusi wakifanikiwa kufikia kiwango cha udhibiti wa virusi mwilini. Amesema katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa mradi huo, vituo 147 vya kutolea huduma na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU (CTC) vimeendelea kutoa huduma, huku jumla ya wananchi 71,149 wakifikiwa na huduma za matibabu. Hata hivyo, Dkt. Mzaga amebainisha kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya watu wanaogundulika kuwa na maambukizi mapya wakiwa katika hatua ya ugonjwa, hali inayohitaji kuimarishwa kwa elimu na tahadhari ili kuzuia maambukizi zaidi. Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewataka waganga wakuu wa halmashauri kuendeleza kampeni za elimu na uhamasishaji kwa wananchi ili kudhibiti maambukizi mapya na kulinda mafanikio yaliyopatikana. Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, wakiwemo Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), imefanya juhudi kubwa kupunguza kasi ya maambukizi, hivyo wataalamu wa afya wanapaswa kuhakikisha hatua zilizofikiwa zinaendelezwa ili kufikia lengo la asilimia 95-95-95 ifikapo mwaka 2030. Aidha, amesisitiza kuwa vitendea kazi vilivyokabidhiwa vinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuimarisha huduma za kinga, upimaji na matibabu ya VVU mkoani humo. Ameagiza waganga wakuu wa halmashauri kufuatilia kwa karibu watu wanaobainika kuwa na maambukizi ili kuhakikisha wanapata huduma stahiki na kuendelea na matibabu, huku akisisitiza umuhimu wa kupinga unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na VVU.

Tue, 17 Nov 2026 20:40:58 +0000
Uncategorized · Issa Michuzi

ECOBANK TANZANIA YAIMARISHA USHIRIKIANO NA SHULE BINAFSI KUPITIA HUDUMA MAALUM ZA KIFEDHA

Ecobank Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano na Taasisi za elimu nchini kwa kuweka mikakati ya kutoa suluhisho za kifedha zinazolenga kusaidia shule binafsi kukua na kujiendesha kwa uendelevu, ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kupanua huduma za kifedha katika sekta ya elimu. Katika kuendeleza mkakati huo, benki hiyo imeandaa mkutano maalumu wa kifungua kinywa kwa Wakurugenzi Wakuu na viongozi wa shule binafsi (Private School CEOs’ Breakfast on Sustainable School Finance), uliofanyika Novemba 16, 2026, katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, uliowakutanisha viongozi wa Taasisi za elimu na wadau mbalimbali kujadili mikakati ya upatikanaji wa fedha na ukuaji endelevu wa shule. Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Dkt. Charles Asiedu, alisema mpango huo ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kuimarisha ushirikiano na taasisi za elimu nchini kwa kuelewa mahitaji yao ya kifedha na kutoa huduma zinazozingatia mazingira na uwezo wa kila shule. Alisema Ecobank inalenga kupanua ushirikiano na shule nyingi zaidi nchini kupitia vyama mbalimbali vya wamiliki na waendeshaji wa shule, akieleza kuwa mawasiliano ya karibu na viongozi wa shule yataisaidia benki kubuni suluhisho za kifedha zitakazochochea ukuaji, kuongeza ufanisi wa uendeshaji na kuhakikisha taasisi hizo zinaendelea kuwa endelevu. Kupitia huduma maalumu za kifedha kwa sekta ya elimu (Education Financial Services), Ecobank inatoa suluhisho mbalimbali zikiwemo mikopo ya ujenzi na upanuzi wa madarasa, maabara, maktaba na mabweni; ufadhili wa ununuzi wa mabasi ya shule, kompyuta na vifaa vya kufundishia; mitaji ya kuendesha shughuli za kila siku; pamoja na huduma za kidijitali za ukusanyaji wa ada na usimamizi wa fedha. Aidha, benki hiyo inatoa huduma za kibenki kwa wafanyakazi wa shule ili kuwawezesha kupata huduma zinazochangia ustawi wao wa kifedha. Dkt. Asiedu alisisitiza kuwa Ecobank haitaki kuwa mtoa huduma za kibenki pekee, bali mshirika wa kimkakati wa taasisi za elimu katika kutekeleza mipango yao ya maendeleo. Aliwahimiza wamiliki na wasimamizi wa shule kushirikiana na benki zao mapema kwa kueleza mipango ya upanuzi na uwekezaji wanaokusudia kufanya ili kupata suluhisho zinazolingana na mahitaji na uwezo wao wa kifedha. Aidha, mkutano huo umefanyika wakati sekta ya elimu nchini ikijiandaa na mabadiliko yanayotarajiwa katika idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule, yakiwemo makadirio ya kundi kubwa la wanafunzi wanaotarajiwa kuingia katika mfumo wa elimu mwaka 2028 (double cohort). Hali hiyo inatarajiwa kuongeza mahitaji ya miundombinu, vifaa vya kujifunzia na uwezo wa shule kutoa huduma bora, hivyo kuhitaji mipango madhubuti ya kifedha. Kupitia mpango huo, Ecobank inalenga kuendelea kushirikiana na wadau wa elimu kujenga shule imara na endelevu zitakazochangia maendeleo ya elimu na uchumi wa Tanzania. Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Dkt. Charles Asiedu akizungumza na Wakurugenzi Wakuu na viongozi wa shule binafsi (Private School CEOs’ Breakfast on Sustainable School Finance) kwenye mkutano maalum uliofanyika Novemba 16, 2026 jijini Dar es Salaam. Baadhi ya wafanyakazi wa Ecobank Tanzania pamoja na Wakurugenzi Wakuu na viongozi wa shule binafsi (Private School CEOs’ Breakfast on Sustainable School Finance) wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Dkt. Charles Asiedu. Picha ya pamoja

Wed, 18 Nov 2026 05:47:33 +0000
Uncategorized · Issa Michuzi

RAIS SAMIA KUFANYA ZIARA YA KITAIFA NCHINI UGANDA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,  akiondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam, kuelekea Entebbe nchini Uganda kwa ajili ya Ziara ya Kitaifa, tarehe 18 Novemba, 2026.

Wed, 18 Nov 2026 08:01:09 +0000
National · Issa Michuzi

WAZIRI MKUU ACHANGISHA BIL. 1.5 UJENZI OFISI YA BAKWATA TABORA.

▪️Rais Samia achangia milioni 200, asifu mchango wa taasisi za dini katika maendeleo ya taifa. WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amefanikisha kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.547 katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Ofisi za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mkoa wa Tabora. Harambee hiyo imefanyika Jumanne, Novemba 17, 2026 katika ukumbi wa Muungano, Mkoani Tabora, ambapo ameipongeza BAKWATA kwa maono ya ujenzi wa Ofisi hiyo. Akizungumza katika harambee hiyo, Dkt. Mwigulu amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye katika harambee hiyo amechangia shilingi milioni 200, anaunga mkono jitihada zinazofanywa na madhehebu ya dini na anathamini mchango wao katika ustawi wa taifa. Amesema kuwa Rais Dkt. Samia anatambua kuwa taasisi za dini zimekuwa mshirika muhimu wa serikali katika malezi, kuimarisha maadili katika jamii na utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu. Dkt. Mwigulu amesema kuwa mchango huo umeifanya Tanzania kuendelea kuwa mfano wa amani barani Afrika na duniani kote. “Palipo na mshikamano, umoja, utulivu, amani na uzalendo, ni dhahiri nchi inaweza kupiga hatua, na wananchi wake wanaweza kupiga hatua”. Amesema kuwa kwa zaidi ya nusu karne, BAKWATA imeendelea kuwa taasisi muhimu katika ujenzi wa taifa mbali na jukumu lake la msingi la mafundisho ya kidini. “BAKWATA imeendelea kuwa mshirika wa karibu wa masuala ya msingi nchini, hasa kwa kuzingatia maadili, uzalendo, na mshikamano” Amesisitiza kuwa maendeleo ya taifa lolote hayapimwi tu kwa kila mmoja kuwa na maendeleo yake binafsi au miundombinu pekee, lakini yanapimwa pia kwa kiwango cha maadili, mshikamano uliopo katika taifa husika. “Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amenituma niwahakikishie kuwa serikali anayoiongoza itaendelea kuheshimu na kuenzi mshikamano kati ya Serikali na taasisi zetu za dini," amesisitiza Dkt. Mwigulu. Akisoma taarifa ya Mradi wa ujenzi wa Ofisi hiyo, Katibu wa Bakwata mkoa wa Tabora, Mohamed Hussein Abeid amesema kuwa ofisi hiyo ambayo itakuwa na ghorofa tano pindi itakapokamilika litagharimu shilingi bilioni 1.8. “Jengo hili litakapokamilika litakuwa na Ofisi za Baraza na Taasisi zake, maduka ya biashara, Ofisi za kupangisha kwa taasisi mbalimbali, ukumbi wa mikutano, sehemu ya kupumzikia kwa ajili ya viongozi wakuu wa baraza na wageni wengine, ujenzi wa jengo hili unategemea kukamilika ndani ya miezi 18”.

Wed, 18 Nov 2026 08:06:26 +0000
Uncategorized · Issa Michuzi

DC SHAKA AKABIDHI VIWANJA 340 KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO TINDIGA

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amekabidhi viwanja 340 vya makazi kwa wahanga wa mafuriko katika Kata ya Tindiga, katika hafla iliyofanyika Kijiji cha Malui. Akizungumza katika hafla hiyo, Shaka amebainisha kuwa pamoja na viwanja hivyo vya makazi, Serikali pia imetenga maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii katika eneo hilo lililotengwa kwa ajili ya wahanga hao. Amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha wahanga hao wanapata makazi salama na mazingira bora ya kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii. "Baada ya mafuriko, Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alimtuma Mhe. Waziri Mkuu Mwigulu kuja kutoa pole kwa wahanga na alihakikisha huduma zote za kibinadamu zinapatikana. Lakini Mhe. Rais Samia alielekeza kutafutwa maeneo ya Serikali ili tuwahamishe mabondeni kule. Leo maelekezo ya Rais Dkt. Samia yametimia, tuko hapa kuyatekeleza kwa vitendo." Alisema Shaka Hata hivyo, Shaka amewataka waliopokea viwanja hivyo kuvitumia kwa ajili ya makazi kama ilivyokusudiwa, akisisitiza kuwa hawaruhusiwi kuviuza viwanja hivyo. Katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya amekabidhi Hati za Umiliki wa viwanja hivyo kwa wahanga hao, na kuongeza kuwa Serikali inaendelea kufanya tathmini ili kuwabaini wahanga wengine wenye uhitaji ili nao waweze kupatiwa viwanja.

Wed, 18 Nov 2026 08:10:29 +0000
Uncategorized · The Citizen

How land rights, savings groups help women rebuild livelihoods

Read the full report from the original source.

Recently
Uncategorized · The Citizen

Belly fat is not always about what you eat, experts explain

Read the full report from the original source.

Recently
Uncategorized · The Citizen

The 5km walk: Why 78 percent of Uyui households lack water

Read the full report from the original source.

Recently
Uncategorized · The Citizen

Tanzania now retains seat at ITU’s governing council

Read the full report from the original source.

Recently
Uncategorized · The Citizen

Key mining conference to focus on value addition

Read the full report from the original source.

Recently
Uncategorized · Business Daily

Borrower allowed to sue Stanbic over negative CRB listing after auction

Read the full report from the original source.

Recently
Uncategorized · Business Daily

She moved to Nigeria for love; Now she makes money helping Kenyans settle there

Read the full report from the original source.

Recently
Uncategorized · The Citizen

Stakeholders outline long-term solutions to Uyui water shortages

Read the full report from the original source.

Recently
Uncategorized · Business Daily

Non-interest income lifts Equity profit to Sh68bn

Read the full report from the original source.

Recently
Uncategorized · The Citizen

Flight disruptions raise fresh doubts over airline reliability

Read the full report from the original source.

Recently
Uncategorized · Business Daily

US inflows now less than half diaspora cash after Sh43bn dip

Read the full report from the original source.

Recently

Page 176 of 1137 · 22731 stories